Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa kushirikisha zaidi watu wa asili

Umoja wa Mataifa kushirikisha zaidi watu wa asili

Umoja wa Mataifa unatarajiwa kuanzisha mkakati wa kushirikisha zaidi watu wa jamii za asili kwenye shughuli za Umoja huo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametangaza hilo leo wakati wa uzinduzi wa mkutano wa 15 wa mjadala wa kudumu kuhusu watu wa jamii za asili unaofanyika wiki hii mjini New York.

Zaidi ya wawakilishi 1,000 wa jamii za watu wa asili wanahudhuria mkutano huo unaozingatia mwaka huu amani na usalama.

Katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa ajili ya mkutano huo, Bwana Ban amesema watu wa asili wanazidi kuathirika na madhara ya mizozo inayohatarisha ardhi yao, rasilimali na haki zao.

(Sauti ya Bwana Ban)

“Amani ya kudumu inatakiwa, watu wa jamii asili waweze kupata haki za kitamaduni, kijamii na kiuchumi. Mkutano wa mwaka 2014 kuhusu watu wa jamii za asili umeuomba Umoja wa Mataifa kuhakikisha mkakati madhubuti. Kwa hiyo tumeandaa mpango kazi kwa ngazi ya muundo mzima, tutakaozindua leo.”

Kwa upande wake Rais wa Baraza Kuu Mogens Lykketoft amesema Baraza hilo limeanzisha mijadala kuhusu mkakati huo ambao utapitishwa rasmi na Baraza Kuu mwezi Septemba mwaka huu.