Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNVIM yaanza kazi kurahisisha usafirishaji bidhaa Yemen

UNVIM yaanza kazi kurahisisha usafirishaji bidhaa Yemen

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha uzinduzi rasmi wa utendaji wa chombo cha umoja huo cha kuthibitisha usafirishaji wa bidhaa za huduma na kibiashara nchini Yemen, UNVIM, kwa mujibu wa azimio la baraza la usalama namba 2216 la mwaka 2015.

Katika taarifa yake, Ban amesema chombo hicho kitarahisha usafirishaji wa bidhaa hizo haraka na bila upendeleo kutoka bandari zisizo chini ya usimamizi wa serikali ya Yemen.

Amesema kuwa UNVIM ni sehemu ya jitihada pana za kuhakikisha misaada ya kibinadamu inafikia wananchi wa Yemen, akitumai kuwa itawezesha kufikiwa kwa suluhu la kisiasa kupitia mazungumzo yanayoendelea huko Kuwait kati ya pande kinzani za Yemen.

UNVIM ina makao yake makuu nchini Djibout na Katibu Mkuu ameshukuru Umoja wa Ulaya, Uholanzi, New Zealand na Marekani kwa mchango wao katika kufanikisha kuanzishwa kwa chombo hicho.