Watatu zaidi wajipigia debe kuwa Katibu Mkuu

Watatu zaidi wajipigia debe kuwa Katibu Mkuu

Leo Jumatano ya Aprili 13, wagombea watatu zaidi wa wadhfa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wamewasilisha hoja zao, wakijipigia debe na kuhojiwa na wawakilishi wa nchi wanachama katika moja ya kumbi za Baraza Kuu la Umoja huo.

Yote hayo ni katika mchakato wa kihistoria na ulio wazi wa kumtafuta mrithi wa Ban Ki-moon, ambaye atahitimisha muhula wake mwishoni mwa mwaka huu, 2016.

image
Danilo Türk, kutoka Slovenia.(Picha:UM/Mark Garten)
Wa kwanza kuwasilisha mtazamo wake kuhusu uongozi wa Umoja wa Mataifa katika miaka mitano baada ya Ban, amekuwa ni Danilo Türk, kutoka Slovenia, ambaye amesema kuna umuhimu wa kuimarisha ubia baina ya Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda, asasi za kiraia, wafanya biashara, na vyombo vya habari.

“Umoja wa Mataifa hufanya kazi katika muktadha ambapo jumuiya za kikanda zimepata umuhimu mkubwa na kutunga sera zao na kuendeleza maarifa yao kufikia upeo mpya. Huu wote ni ubia ambao Umoja wa Mataifa unapaswa kukuza, na ambapo Katibu Mkuu anapaswa kuchangia. Na hili linaenda sanjari na maeneo yote matatu ya kazi ya Umoja wa Mataifa: kudumisha amani na usalama, maendeleo endelevu na haki za binadamu.”

image
Vesna Pusić, Naibu Waziri Mkuu wa kwanza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Croatia akihutubia Baraza Kuu katika kugombea nafasi ya Katibu Mkuu. Picha: UM/Rick Bajornas
Wa pili kuwasilisha hoja na mtazamo wake amekuwa ni Dkt. Vesna Pusić, kutoka Jamhuri ya Croatia. Dkt. Pusić amesema ili kushughulikia malengo asili ya Umoja wa Mataifa, usimamizi wa umoja huo ni suala muhimu sana

“Umoja huu usipofanya kazi vyema, amani, maendeleo, usaidizi wa kibinadamu, haki za binadamu, miradi yote ya elimu na maendeleo tunayojali na kutaka kushughulikia vitasalia kuwa ndoto tu, kwani umoja huu utakuwa haufanyi kazi ipasavyo. Mifumo rahisi na masuluhu rahisi ni vitu vinavyoweza kuleta mafanikio zaidi.”

image
Bi Natalia Gherman, kutoka Jamhuri ya Moldova.(Picha:UN/Webcast/video capture)
Wa mwisho kuzungumza leo, amekuwa ni Bi Natalia Gherman, kutoka Jamhuri ya Moldova, akitilia msisitizo usalama, maendeleo na haki za binadamu

“Hakuna usalama bila maendeleo, na hakuna maendeleo bila usalama, na hakuna lolote bila kuheshimu haki za binadamu. Na Umoja wa Mataifa ni lazima ujitahidi zaidi ili kutimiza ahadi za ubia mpya wa kimataifa kwa ajili ya raia wa ulimwengu. Umoja wa Mataifa unaweza kusaidia nchi wanachama kutimiza ahadi hizi; una jukumu la aina yake la kufanya hivyo.”

Hapo kesho Alhamisi ya Aprili 14, Baraza Kuu litawasikiliza na kuwahoji wagombea wengine watatu, kama sehemu ya mchakato huo ambao utaendelea hadi pale atakapoteuliwa Katibu Mkuu mpya.