Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano yafikiwa kuhusu kuwezesha usaidizi wa kibinadamu Syria

Makubaliano yafikiwa kuhusu kuwezesha usaidizi wa kibinadamu Syria

Wanachama wa kundi la kimataifa kuhusu usaidizi kwa Syria, wamekubaliana leo kuhusu kuhakikisha usaidizi wa kibinadamu unawafikia wahitaji, uhasama unasitishwa na kuendeleza jitihada za mpito wa kisiasa. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano wa siku mbili uliomalizika leo mjini Munich, Ujerumani, ambako wadau hao wameamua kuwa ufikishwaji misaada kwa maeneo yalozingirwa nchini Syria utaanza wiki hii, na kwamba katika muda wa wiki moja, kikosi kazi cha kundi hilo la kimataifa kitatoa mwongozo kuhusu jinsi ya kusitisha uhasama kote nchini Syria ili kuwezesha shughuli za kibinadamu.

Tayari kikosi kazi hicho cha kimataifa kimeanza kukutana mjini Geneva, Uswisi, kikiongozwa na Jan Egeland, Mshauri Mkuu wa Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura.

Kwa kauli moja, wanachama wa kundi hilo wameeleza dhamira yao kuwezesha mara moja utekelezaji kikamilifu wa azimio la Baraza la Usalama namba 2254, ambalo lilipitishwa mnamo Disemba 18, 2015, ambalo linataka uwepo mpito wa kisiasa unaomilikiwa na kuongozwa na Wasyria wenyewe, kukomesha mashambulizi holela na kuwezesha usaidizi wa kibinadamu.