Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rwanda na UNIDO zasaini makubaliano kuhusu programu ya kitaifa

Rwanda na UNIDO zasaini makubaliano kuhusu programu ya kitaifa

Shirika la Umoja wa Mataifa la Viwanda na Maendeleo, UNIDO, limesaini makubaliano na Rwanda kuhusu programu ya kitaifa, ambayo inatarajiwa kupanua uchumi wa Rwanda na kuongeza nafasi za ajira.

Programu hiyo itaangazia sera ya viwanda na usaidizi kwa maeneo maalum ya uchumi, uongezaji thamani kwa bidhaa za kilimo na usindikaji wa vyakula, kuendeleza nguvu kazi kwa ukuaji wa viwanda na uchumi, usimamizi wa mazingira, na nishati.

Makubaliano hayo yamesainiwa mwishoni mwa ziara ya siku mbili ya Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, Li Yong nchini Rwanda, ambako amejadili na Rais Paul Kagame kuhusu usaidizi wa UNIDO kwa Rwanda, na jinsi ya kuiendeleza nchi hiyo kwenye mkondo wa maendeleo jumuishi na endelevu ya viwanda.

Bwana Li amemsifu Rais Kagame na uongozi wake, na hatua dhahiri zilizopigwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini humo, akiitaja Rwanda kuwa mfano wa kuigwa na nchi zingine za Afrika katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi.

Kati ya mwaka 2006 na 2012, uchumi wa Rwanda umekuwa kwa kiwango cha wastani wa asilimia 8.2, na asilimia 5.9 ya ukuaji mnamo mwaka 2014.