Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

#Burundi yazidi kumtia hofu Ban, kadhalika Madaya #Syria

#Burundi yazidi kumtia hofu Ban, kadhalika Madaya #Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amerejelea kauli yake kuhusu ukosefu mkubwa wa utulivu nchini Burundi, sanjari na hali isiyotabirika.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu mipango yake ya utekelezaji kwa mwaka huu wa 2016, Ban amesema hofu zaidi ni kwamba ghasia zinaweza kuenea zaidi nchini humo na kuvuka mipaka.

Kwa mantiki hiyo amesema…

(Sauti ya Ban)

“Serikali lazima ichukue hatua kujenga imani ikiwemo kuwaachia huru wafungwa wanaoshikiliwa kwa imani na misimamo yao na iondoe vikwazo dhidi ya mashirika ya kiraia. Kwa hiyo basi naunga mkono na kupongeza ziara ya wiki ijayo ya Baraza la Usalama nchini Burundi pamoja na jitihada za Muungano wa Afrika.” 

Ban amesema jamii ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua zote ili kumaliza mkwamo wa kisiasa na kuepusha janga la kibinadamu.

Kuhusu hatma ya Madaya huko Syria ambako raia kwa mara ya kwanza tangu mwezi Oktoba wamepata msaada wa chakula Ban amesema matumizi ya njaa kama silaha ya vita ni uhalifu kwa hiyo..

(Sauti ya Ban) 

“Pande zote ikiwemo serikali ya Syria ambayo ina wajibu mkuu wa kulinda wasyria, zinatekeleza uhalifu huu na vitendo vingine vya kikatili vilivyopigwa marufuku na sheria za kimataifa za kibinadamu.”