Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukuaji uchumi duniani kudhoofika, lakini hali shwari: Ripoti

Ukuaji uchumi duniani kudhoofika, lakini hali shwari: Ripoti

Ukuaji dhaifu wa uchumi katika nchi zinazoibuka kiuchumi utakuwa na madhara katika ukuaji wa uchumi duniani kwa mwaka huu wa 2016.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya mwezi huu ya Benki ya dunia kuhusu matarajio ya uchumi duniani.

Hata hivyo ripoti imesema licha ya hali hiyo, kasi ya ukuaji uchumi duniani itaongezeka na kuwa asilimia mbili nukta tisa ikilinganishwa na asilimia Mbili nukta Nne mwaka jana kutokana na nchi tajiri kushika kasi kiuchumi.

Ripoti imesema kasi ndogo ya ukuaji uchumi kwa nchi zinazoibuka itaathiri nchi zinazoendelea na hivyo kutishia mafanikio yaliyopatikana na kukwamua watu kutoka lindi la umaskini.

Ukuaji uchumi katika nchi zinazoendelea unatarajiwa kukua kwa asilimia nne nukta Nane mwaka huu ikiwa ni kiwango kidogo kuliko matarajio.

Akizungumzia ripoti hiyo Makamu Rais wa Benki ya dunia na mchumi mkuu wa taasisi hiyo Kaushik Basu amesema suluhu pekee ni kuweka sera bora za kifedha na za benki kuu ili kupunguza athari na kusaidia ukuaji uchumi.