Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban atoa ujumbe wa amani kwa Siku ya Uhuru Sudan Kusini

Ban atoa ujumbe wa amani kwa Siku ya Uhuru Sudan Kusini

Wakati taifa la Sudan Kusini likijiandaa kuadhimisha miaka mitatu tangu kujinyakulia uhuru mnamo Julai 9, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema viongozi wa taifa hilo changa zaidi wana wajibu wa kuumaliza mgogoro uliopo sasa, ambao amesema umebuniwa na mwanadamu.

Katika taarifa iliyosomwa na msemaji wake, Bwana Ban amekumbusha kuhusu matumaini na matarajio ya watu wa Sudan Kusini kwenye siku ya uhuru wao mnamo Julai 9 mwaka 2011, na kusema kwamba matumaini hayo yalisambaratishwa na mgogoro huo uliolipuka mnamo Disemba mwaka 2013. Amesema watu wa Sudan Kusini wanaathiriwa na mapigano, maelfu yao wakiwa wameuawa, huku ukatili ukitekelezwa dhidi ya raia kwa sababu viongozi wao wameshindwa kukomesha mapigano.  Stephane Dujarric ni Msemaji wa Katibu Mkuu

“Zaidi ya watu milioni 1.3 wamelazimika kuhama makwao, na ufadhili usipotolewa na pande husika kushirikiana, mamilioni ya maelfu ya watu wanakabiliwa na hatari ya njaa katika miezi ijayo. Katibu Mkuu anawakumbusha viongozi wa Sudan Kusini kuwa hili ni tatizo lililoletwa na mwanadamu. Ni wajibu wao, na wana mamlaka ya kulimaliza. Amewataka watimize matarajio ya watu wao, kuweka chini silaha na kurejea mara moja kwa meza ya mazungumzo.”

Katibu Mkuu pia amewahakikishia watu wa Sudan Kusini kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kusimama nao bega kwa bega, na kuendelea kufanya juhudi zote kuwapa ulinzi na usaidizi wa kibinadamu ambao ni haki yao.