Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laahidi hatua kali kufuatia madai ya jaribio la nyuklia DPRK

Baraza la Usalama laahidi hatua kali kufuatia madai ya jaribio la nyuklia DPRK

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamelaani vikali jaribio la nyuklia lililofanywa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, DPRK, leo Jumatano ya Januari 6, kufuatia kikao kikao cha dharura walichokuwa nacho leo kushughulikia suala hilo nyeti.

Taarifa ya Baraza la Usalama ilotolewa na Msemaji wa Katibu Mkuu imesema kuwa jaribio hilo la DPRK ni ukiukwaji dhahiri wa maazimio ya Baraza hilo namba 1718 (2006), 1874 (2009), 2087 (2013), na 2094 (2013) na kanuni ya kutoeneza silaha za nyuklia, na hivyo ni tishio bayana kwa amani na usalama wa kimataifa.

Wajumbe hao pia wameelezea azma yao ya awali ya kuchukua kila hatua kali zaidi iwapo DPRK ingefanya jaribio jingine la nyuklia. Kwa mantiki hiyo, wamesema wataanza mara moja kazi ya kuchukua hatua hizo, katika azimio jipya la Baraza la Usalama.