Matarajio ya mazao yapungua sababu ya El-Niño kusini mwa Afrika

Matarajio ya mazao yapungua sababu ya El-Niño kusini mwa Afrika

Ongezeko la joto na ukosefu wa mvua uliosababishwa na El-Niño unatarajia kuathiri mazao na mifugo kusini mwa Afrika mwaka 2016.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Shirika la Chakula na Kilimo FAO, ambalo limeongeza kwamba msimu wa kupanda mahindi umeshaanza kwenye ukanda huo lakini ardhi imekosa maji ya kutosha.

FAO imeeleza kwamba El-Niño inathiri zaidi wakulima wadogo wadogo ambao hutegemea zaidi mvua kwa ajili ya kilimo.

Aidha ripoti ya FAO inaonyesha kwamba mvua zinatarajia kuendelea kuadimika hadi mwezi Machi mwaka ujao kwenye ukanda huo na hivyo kusababisha ukame kwenye nchi kadhaa zikiwemo Afrika Kusini, Lesotho na Swaziland.

Tayari bei za mahindi zimeongezeka kwa asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka uliopita kwa sababu ya msimu mbaya wa kilimo, FAO imesema.

Usaidizi wa FAO unalenga kupunguza athari za ukame huo, na pia kuwajengea wakulima wadogo wadogo uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.