Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi yamulikwa Ban akizungumzia matukio ya 2015

Burundi yamulikwa Ban akizungumzia matukio ya 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amekuwa na mkutano wa mwisho wa mwaka na wanahabari leo jijini New York, akihutubia kuhusu masuala mseto yaliyoibuka mwaka huu wa 2015, ambapo Umoja huo umeadhimisha miaka 70 tangu kuasisiwa kwake.

Kwanza kabisa, Ban amezungumza kuhusu ufanisi, akianza na Mkataba wa Paris kuhusu Tabianchi, ambao ameutaja kuwa ishara ya matumaini katika nyakati zenye utata.

“Mkataba wa Paris ulizidi matarajio. Mkataba wa Paris unatupatia mpango wa A kwa ajili ya sayari dunia, ambao ni kabambe.”

Aidha, Ban amepongeza hatua nyingine kuu za ufanisi zilizopigwa mwaka huu, zikiwemo kupitishwa kwa malengo 17 ya maendeleo endelevu mwezi Septemba, na Mkakati wa Sendai mwezi Machi kuhusu kupunguza madhara ya majanga.

“Ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu ni mwongozo wetu wa malengo 17 ya kina ya kumaliza umaskini na kujenga jamii zenye amani. Ajenda ya Addis Ababa ya Kuchukua Hatua ni msingi wetu wa ufadhili kwa maendeleo. Mkakati wa Sendai unatuelekeza kuweka uthabiti”

Licha ya hatua hizo za ufanisi, Katibu Mkuu amemulika pia changamoto kuu zilizoughubika mwaka huu, zikiwemo idadi kubwa ya wakimbizi na watu wanaofurushwa ndani ya nchi zao.Ametaja juhudi za kidiplomasia zinazoendelea wiki hii za kutanzua mizozo katika nchi za Libya, Yemen na Syria, kama njia moja ya kupatia suluhu changamoto ya mmiminiko wa wakimbizi

Aidha, Ban amemulika tatizo la ugaidi

“Kupambana tishio linalowekwa na Da’esh, Boko Haram, al-Shabab  na makundi mengine ya kigaidi ni muhimu. Mwezi ujao, nitawasilisha kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mpango wa kuchukua hatua kuzuia itikadi kali katili.”

Na kuhusu mizozo Afrika, Burundi imekuja kwanza

“Nasikitishwa na kuongezeka machafuko Burundi. Tulichoshuhudia siku chache zilizopita kinatisha. Nchi hiyo ipo kwenye hatari ya kutumbukia vita vya wenyewe kwa wenyewe, na hatari ya kuathiri ukanda mzima. Suluhu jumuishi la kisiasa linahitajika kwa dharura. Ni lazima tufanye kila tuwezalo kuzuia ukatili wa halaiki, na kuchukua hatua madhubuti iwapo utaibuka”

Ban amegusia pia hali Sudan Kusini, akisema kuwa ingawa Umoja wa Mataifa kupitia operesheni zake za amani unaedelea kuwapa hifadhi watu 185,000, hiyo haiwezi kuwa suluhu ya kudumu, akitoa wito kwa pande kinzani kuweka taasisi za mpito kabla mwisho wa mwezi Januari.