Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 95 ya wakazi wa dunia wana simu za mkononi:ITU

Asilimia 95 ya wakazi wa dunia wana simu za mkononi:ITU

Shirika la mawasiliano duniani, ITU limetoa ripoti yake kuhusu maendeleo ya matumizi ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano, TEHAMA ikionyesha ongezeko la matumizi ya mitandao ya intaneti na simu za mkononi.

Ripoti hiyo ikiangazia kipindi cha miaka kumi tangu mwaka 2005, imezinduliwa leo ikisema kwa sasa zaidi ya watu Bilioni Saba, sawa na asilimia 95 ya wakazi wote duniani wamejisajili kutumia simu za mkononi ikilinganishwa na watu Bilioni Mbili nukta Mbili mwaka 2005.

Halikadhalika watu Bilioni Tatu nukta Mbili sawa wanapata huduma ya mtandao ikilinganishwa na watu Bilioni 2.2 katika kipindi hicho hicho.

ITU inasema takwimu hizo ni habari njema lakini bado hatua zaidi zahitajika kwenye nchi maskini ambako TEHAMA inaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa kusaidia watu kuondokana na umaskini uliokithiri.

Jaroslaw Ponder ni mratibu wa ITU kwa ukanda wa Ulaya

(Sauti ya Brahima)

“Jamii ya kimataifa inapaswa kupatia kipaumbele suala la kuondoa tofauti ya upatikanaji wa TEHAMA kati ya nchi maskini na zile tajiri. Kwa sasa upatikanaji wa intaneti uko zaidi kwa nchi zilizoendelea huku zile zinazoendelea, LDCs zikisalia nyuma.”

Ripoti hiyo imeangazia matumizi ya TEHAMA katika nchi 167 ambapo Korea Kusini inashika nafasi ya kwanza katika maendeleo ya TEHAMA huku Kenya ikiwa nafasi ya 124, Uganda 149, Tanzania nafasi ya 157 huku nafasi ya mwisho kabisa ikishikiliwa na Chad.