Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lalaani mauaji ya raia yaliyofanywa na ISIL

Baraza la Usalama lalaani mauaji ya raia yaliyofanywa na ISIL

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali mauaji ya kikatili ya raia wawili wa China na Norway yaliyofanywa na kikundi cha kigaidi cha ISIL.

Katika taarifa yao wajumbe hao wamesema uhalifu huo dhidi ya Fan Jinghui kutoka China na Ole Johan Grimsgaard-Ofstad wa Norway unadhihirisha ukatili wa ISIL, kundi ambalo linawajibika na maelfu ya vitendo vya uhalifu dhidi ya watu wa imani zote za kidini, kabila na utaifa.

Wametuma rambirambi zao kwa familia za raia hao pamoja na serikali za China na Norway huku wakitaka wahusika wa kitendo hicho wafikishwe mbele ya sheria.

Halikadhalika wamesisitiza kuwa kikundi cha ISIL ni lazima kitokomezwe na kwamba itikadi ya ukosefu wa stahmala na ghasia ambayo inapigiwa chepuo na kikundi hicho ni lazima ifutike.

Wamesisitiza kuwa kitendo cha ISIL kuendelea na ukatili wake, hakikatishi tamaa baraza hilo bali kinaimarisha harakati na azma ya kuungana zaidi kutokomeza vitendo hivyo.