Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumo waimarishwa kubaini kiwango cha hewa ya ukaa:FAO

Mfumo waimarishwa kubaini kiwango cha hewa ya ukaa:FAO

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema mfumo ulioboreshwa wa kubaini ukubwa wa misitu, ujazo wa hewa ya ukaa kwenye miti na uwezo wake kuvuta hewa hiyo utasaidia nchi kuwa na picha kamili ya hewa hiyo katika misitu kuliko ilivyokuwa awali.Taarifa kamili na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Mfumo huo wa kwenye kompyuta uitwao GlobAllomeTree unasaidia wanasayansi, wahifadhi misitu, kampuni binafsi na watunga sera kuboresha tathmini za uchukuaji takwimu hizo na hatimaye kuwa na kiwango sahihi cha gesi chafuzi kinachopaswa kupunguzwa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Afisa misitu wa FAO Matieu Henry amesema kushindwa kupata takwimu sahihi kuhusu hali halisi ya misitu ni moja ya vikwazo vya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia sekta ya misitu.

Kwa mantiki hiyo amesema mfumo wa sasa ulioboreshwa utawezesha nchi kuchukua uamuzi sahihi kwa kuwa zitafahamu kiwango cha hewa ya ukaa kwenye miti na kiwango kinachopunguzwa kwa hewa chafuzi kunyonywa na miti hiyo.

FAO imesema nchini Tanzania, wadau wanashirikiana na FAO kukusanya takwimu kupitia mfumo huo ambao ule wa kwanza kabisa ulizinduliwa mwaka 2013.