Utaifa na madhila kwa watoto: UNHCR
Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kunafanyika mjadala kuhusu umuhimu wa utaifa duniani wakati huu ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limetoa ripoti yake mpya inayoeleza kuwa watoto wasio na utaifa kote duniani wana hisia zinazofanana za kubaguliwa, kuvunjika moyo na kukata tamaa. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.
(Taarifa ya Assumpta)
Kamishna Mkuu wa UNHCR, António Guterres, amesisitiza kuwa ripoti hiyo ambayo imetolewa mwaka mmoja baada ya kuzinduliwa kwa kampeni ya kutokomeza kutokuwa na utaifa ifikapo mwaka 2024 iitwayo #IBelong, inamulika haja ya kukomesha taabu ya watoto wanaokosa utaifa katika dunia ambapo mtoto mmoja huzaliwa bila utaifa kila dakika kumi.
Kwa mantiki hiyo, UNHCR imeonya kuwa hatua za dharura zinahitajika kuchukuliwa mapema kabla kitendo cha watoto kutokuwa na utaifa hakijawatumbukiza kwenye jinamizi ya taabu.
Artee Mayer ni mmoja wa watoto huko Thailand asiye na utaifa na anafikiria hatma yake.
(Sauti ya Artee)
“Kama mimi na wenzangu hapa shuleni tukiwa na utaifa, maisha yatakuwa mazuri kwa kila mtu; kutoka giza kuwa nuru, machungu kuwa matumaini kama anga lenye nuru. Tunaweza kuendelea na masomo na kufikia ndoto zetu.”