Sensa ya kilimo kufanyika mwakani:FAO
Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limetangaza kuwa sensa mpya ya kilimo itaanza mwakani kwa lengo la kukusanya taarifa na takwimu kuhusu sekta hiyo ulimwenguni kote.
Ili kufanikisha mchakato huo, FAO imetoa mwongozo wa kusaidia serikali katika mpango huo, muongozo ambao unaendana na mahitaji na uwezo wa nchi husika, ikiwa ni mwongozo unaotolewa na shirika hilo kila baada ya miaka 10.
Kiongozi wa masuala ya sensa ndani ya FAO, Jay Castano amesema shughuli hiyo itatoa taswira halisi ya sekta ya kilimo duniani ikiwemo ukubwa wake, matumizi ya ardhi, eneo lililopandwa mazao, vifaa vya umwagiliaji na matumizi ya pembejeo za kilimo na sensa ya sasa ni tofauti..
(Sauti ya Castano)
“Sensa za kilimo hapo awali zilihusisha mazao na mifugo na wakati mwingine kilimo cha mazao ya majini ilipohitajika. Lakini sensa yasa tumeongeza uvuvi na gesi chafuzi zitokazo kwenye kilimo na athari zake kwenye mazingira.”
Bwana Castano amesema matumizi ya muongozo wa sasa yatawezesha matokeo ya sensa kutambulika kimataifa na hata nchi kujipima maendeleo ya sekta yao na nchi nyingine.