Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mvua zaharibu makazi ya waishio mabondeni huko Somalia: OCHA

Mvua zaharibu makazi ya waishio mabondeni huko Somalia: OCHA

Maeneo ya kaskazini mwa Somalia na kando mwa mabonde ya mto Shabelle yamekumbwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa zilizoanza kunyesha mwanzoni mwa mwezi huu.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na usaidizi wa kibinadamu, OCHA imesema maelfu ya watu wanaoishi kwenye mabondeni wamepata madhara makubwa kwa kupoteza makazi yao ambapo hadi sasa watoa huduma wanatathmini kiwango cha madhara.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Somalia, Peter de Clercq amesema hali ya sasa inatia wasiwasi kutokana na El Niño na watu zaidi ya Milioni Tatu wanahitaji misaada ya kuokoa maisha  yao.

Amesema kwa sasa wanahitaji dola Milioni 30 kukidhi mahitaji hayo sambamba na kuweka maandalizi pindi mvua za El Niño zitakapoanza.