Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchangiaji wa sekta ya umma na binafsi katika tabianchi uangaliwe vyema: Ban

Uchangiaji wa sekta ya umma na binafsi katika tabianchi uangaliwe vyema: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema baada  ya kupitishwa kwa malengo ya maendeleo endelevu au ajenda 2030 ya mwezi uliopita kilichosalia sasa ni fedha kwa ajili yakuweza kufanikisha utekelezaji wake.

Akizungumza wakati wa mlo wa mchana na mawaziri wa fedha kuhusu uchangiaji wa sekta ya umma kwa ajili ya tabianchi huko Lima, Peru, Ban amesema ajenda hiyo sambamba na makubaliano mapya mabadiliko ya tabianchi yatakayopitishwa jijini Paris, Ufaransa vitakuwa ni muhimu katika tabianchi yenye kiwango kidogo cha hewa ya ukaa na mazingira yenye manufaa kwa wote.

Hata hivyo Ban amesema changamoto ni uchangishaji fedha, ambapo amesema ni vyema kuamua mfumo wa kuamua uchangiaji wa umma ni upi na jinsi gani uchangiaji wa sekta binafsi kwa masuala ya tabianchi nchi unajumuishwa katika nchi zote zilizoendelea na zile zinazoendelea.

Amesema serikali zinaweza kuchagiza mabadiliko kwa kutunga sera ambazo zinahamasisha sekta binafsi kuachana na ukuaji mfupi wa uchumi na badala yake kuwekeza katika miradi isiyoharibu mazingira na ambayo itastahilimi ukuaji kwa muda mrefu.