Skip to main content

SDG na Mapinduzi ya viwanda Afrika kuangaziwa leo UM

SDG na Mapinduzi ya viwanda Afrika kuangaziwa leo UM

Ikiwa leo ni siku ya pili ya mjadala kuhusu ajenda ya maendeleo endelevu, SDG iliyopitishwa Ijumaa na wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, mikutano mbali mbali ya kando inaendelea na miongoni mwao ni ule unaohusu mkakati wa kuleta mapinduzi ya viwanda barani Afrika.

Akihojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa kuhusu mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda, UNIDO Li Yong amesema ajenda kuu ni kujadili ubia wa jinsi ya kusongesha mbele malengo endelevu barani Afrika, hususan lengo namba Tisa la miundombinu, na mapinduzi ya viwanda jumuishi na endelevu.

Amesema viongozi kutoka nchi 11 za Afrika sambamba na viongozi wa Muungano wa Afrika watashiriki kikao hicho na kwamba..

(Sauti ya Li)

 “Wataeleza ni jinsi gani wanataka kuona mapinduzi ya viwanda yanafikiwa barani humo kwa mujibu wa ajenda 2030. Natumai baada ya mkutano huu muhimu kutakuwepo na nyaraka pengine taarifa ya pamoja au azimio au chochote kile likieleza malengo ambayo wanataka kufikia, au hata linaweza kupelekea kwa hatua zaidi kutoka Baraza kuu, pengine azimio.”