Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yataka viongozi wa Ulaya watimize ahadi zao kuhusu wakimbizi

UNICEF yataka viongozi wa Ulaya watimize ahadi zao kuhusu wakimbizi

Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limekaribisha kuongezeka kwa ahadi kutoka kwa viongozi wa Ulaya za kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji, likisema kwamba ahadi hizo zinapaswa kugeuzwa kuwa hatua za nchi zote wanachama wa EU kuwalinda watoto kikamilifu.

Kufikia sasa, watoto tayari ni robo ya waomba hifadhi barani Ulaya mwaka huu. Katika miezi sita ya kwanza ya 2015, watoto 106,000 waliomba hifadhi katika nchi za Ulaya, wengi wao wakiwa wametokea Syria, Iraq na Afghanistan.

Idadi hiyo ni ongezeko la takriban asilimia 75 kutoka mwaka 2014.

Peter Salama ni Mkurugenzi wa kikanda wa UNICEF, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini..

“Tunapaswa kuhakikisha kuwa katika safari nzima, kutokea wanapoanza safari, nchi wanakopitia na hatimaye hadi katika nchi wanakohamia, watoto wanalindwa kutokana na unyanyasaji, na kuhakikisha kuwa sera zote za utoaji hifadhi zinazingatia maslahi bora ya mtoto.”

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Yoka Brandt, amesema kuwalinda watoto wakimbizi na wahamiaji kutokana na hatari, hususan wakati msimu wa baridi ukikaribia, kunapaswa kuwa kiini cha jitihada za Ulaya, akiongeza kuwa watoto hao tayari wameteseka sana na wana haki ya kulindwa.