Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio dhidi ya watoa misaada huko Darfur lalaaniwa

Shambulio dhidi ya watoa misaada huko Darfur lalaaniwa

Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio lililofanywa na watu wasiojulikana wakiwa na silaha dhidi ya gari lililokuwa limebeba watoa huduma za kibinadamu huko Darfur magharibi nchini Sudan.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini humo Marta Ruedas, amesema katika shambulio hilo dereva na afisa usalama waliuawa ilhali maafisa wawili wa wizara ya afya na daktari kutoka shirika la afya duniani walijeruhiwa.

Amesema shambulio hilo lilitokea kilometa 40 kutoka mji wa Geneina wakati wafanyakazi hao wakirejea kutoka operesheni zao za kawaida za usaidizi na kwamba washambuliaji waliiba gari na kutoweka.

Mratibu huyo amesema matukio kama hayo ya ukosefu wa usalama yanaendelea kukwamisha operesheni za kijasiri zinazofanywa na wafanyakazi wa misaada wakati huu ambapo zaidi ya watu Milioni Mbili na Nusu wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Tangu mwezi Januari mwaka huu kumekuwepo na matukio 131 ya mashambulizi yakihusisha utekaji nyara magari na binadamu huko Darfur, matukio ambayo yameathiri watoa misaada na walinda amani.