Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusipojali mazingira, dunia yetu itaangamia: viongozi wa dini

Tusipojali mazingira, dunia yetu itaangamia: viongozi wa dini

Miezi michache kabla ya mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, wasanii, wanasiasa na viongozi wa jamii na dini wamekutana mjini Paris Ufaransa ili kuonyesha mshikamano wao katika kutunza mazingira. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.(Taarifa ya Grace)

Miongoni mwa washirika wa mkutano huo uitwao "why do I care" Yaani kwanini najali? walikuwa viongozi wa dini kutoka Afrika Mashariki wakiwemo Sheikh Abdalla Kamwana wa Kenya, mchungaji Nathan Kyamaniwa wa Uganda na Askofu Frederick Shoo wa Tanzania Kaskazini.

Askofu Shoo ametumia methali ya kwao inayosema unacheza na moto hadi kibanda kinateketeza.

“ Dunia tunapoishi  ni kama kibanda kikubwa cha kiafrika. Na Mungu ametuweka kila mmoja kwenye nafasi yake. Lakini tumevumbua mchezo wa moto tunaoita soko, linalokuwa na kuendelea kubadhiri mali asili. Mwisho wa siku, kibanda chetu, nyumba yetu, itateketezwa. Swali ni nani ataokolewa? Jibu ni: hakuna hata mmoja.” 

Kwenye ujumbe wake kwa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kila mtu duniani na ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha vizazi vijavyo vinarithi sayari yenye afya nzuri.