Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana 700 wakuna vichwa kuhusu hatma ya SDG’s:

Salina Abraham, Rais wa jumuiya ya kimataifa ya wanafunzi wa masuala ya misitu. Picha: UM/Eskinder Debebe

Vijana 700 wakuna vichwa kuhusu hatma ya SDG’s:

Masuala ya UM

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, kumeanza jukwaa la vijana kutoka nchi wanachama wa umoja huo, wakiweka bayana kile wanachoona ni muhimu kwa mustakhbali wao.

(SAUTI YA SALINA ABRAHAM  CUT)

“Maendeleo endelevu sio kulazimika kuacha nyumba yako, familia yano na utamaduni wako ili kuwapa watoto wako maisha stahiki, maendeleo endelevu sio maefu kwa mamilioni ya Wasyria kukimbia vita na mara nyingi kukutana na vikwazo na kukataliwa, sio kuficha lugha na utamaduni wako katika jitihada za kubadilika na kubaini kamwe hautakubalika. Maendeleo endelevu ni kuweza kuwa na rasilimali, fursa, usalama na nyenzo ili kuunda fursa mpya popote pale utakapochagua kupaita nyumbani.”

Ni kijana Salina Abraham, Rais wa jumuiya ya kimataifa ya wanafunzi wa masuala ya misitu akizungumza akizungumza kwa hisia Kali na kutoa ujumbe mzito  katika ufunguzi wa kongamano la Umoja wa Mataifa la vijana.

Takribani vijana 700 kutoka sehemu mbalimbali duniani wamekutana leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa New York kushiriki kongamano hilo linalofanyika kila mwaka tangu mwaka 2012.

Katika kongamano hilo la siku mbili vijana wanajadili na viongozi wawakilishi wa serikali, asasi za kiraia, na wadau wengine kuhusu será na mikakati bunifu kwa ajili ya kusongesha mbele agenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 au SDG’s.

image
Bi. Marie Chatardová, Rais wa baraza la Umoja wa Mataifa la kiuchumi na kijamii ECOCOS. Picha: UM/Video capture
Marie Chatardová, Rais wa baraza la Umoja wa Mataifa la kiuchumi na kijamii ECOCOS lililoandaa kongamano hilo la vijana amesema ni muhimu sana kuwawezesha vijana ili kuvunja mzunguko wa umasikini na kuwaruhusu kufikia kilele cha uwezo wao, kwani wakipata elimu inayostahilli, elimu, na nyenzo stahiki watajenga jamii bora kwani wana nguvu, ubunifu na werevu wa kupanua wigo wa ujasiriamali na kuunda ajiria kwa ajili yao na wengine.

Akisistiza kuhusu umuhimu huo, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu vijana Jayathma Wickramanayake,amesema

image
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu vijana Jayathma Wickramanayake. Picha: UM/Video capture
(SAUTI YA JAYATHMA WICRAMANAYAKE-1)

“Moja ya changamoto kubwa tunazoziona ingawa tunaendelea kuzungumzia ushiriki hatuoni fursa hiyo , au hatuzioni rasilimali hizo zinazohitajika ili kusukuma suala hili na kuweza kutekeleza tunayonena.”

Naye naibu Katibu Mkuu Bi Amina J. Mohammed ametoa changamoto kwa vijana

image
Naibu Katibu Mkuu Bi Amina J. Mohammed. Picha: UM/Video capture
(SAUTI YA AMINA J MOHAMED)

“Pigeni debe, najua kwanza ajenda hii ilishajihishwa na vijana, ni ajenda ya kimataifa na itakuwa na ugumu , lakini yaliyomo ni muhimu, kuwa na sauti inayosikiliza pande zote, kuondoa ushindani wa rika na kuugeuza kuwa ushirika kwa matokeo ambayo yataleta maisha bora kwa wote kuanzia vijijini, majumbani, hadi kwenye jamii na kuhakikisha wote wamejumuishwa.”

Akizichagiza serikali na jumuiya ya kimataifa kufungua milango vya ushiriki wa vijana bi Wicramanayaye ameongeza

(SAUTI YA JAYATHIMA WICRAMANAYAKE -2)

“Ni lazima tupanue wigo zaidi na kufungua milango iliyofungwa , tuondoe walinzi milangoni, ili kuwaruhusu vijana kushiriki , endapo tunawategemea vijana kubeba mwenge wa ajenda hii. Nadhani kuna haja kubwa ya kutekeleza tunayohubiri, tunazungumzia kutomwacha yeyote nyuma lakini ni dhahiri kwamba tusipotimiza haya vijana wataubakiza nyuma  Umoja wa Mataifa .”

Masuala mengine yanayomulikwa na vijana katika kongamano hilo ni fedha  , teknolojia, kujengewa uwezo na biashara na yatakayojiri mwisho wa kongamano hili yatajumuishwa katika kongamano la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu maendeleo endelevu na pia katika kongamano la Umoja wa Mataifa linalojadili na kutathimini utekelezaji wa SDG’s.