Skip to main content

Baraza la usalama lafanya kikao cha faragha kuhusu Sudan Kusini

Baraza la usalama lafanya kikao cha faragha kuhusu Sudan Kusini

Kuelekea miaka minne ya uhuru wa Sudan Kusini, Baraza la usalama leo jumatano limekuwa na kikao cha faragha kuhusu nchi hiyo ambapo Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Hervé Ladsous amewapatia wajumbe taarifa kuhusu hali ilivyo nchini humo.

Kikao hicho cha faragha kimefanyika huku maelfu ya wananchi wa Sudan Kusini wakiendelea kukumbwa na madhila kutokana na kuendelea kuongezeka kwa mapigano  ya wenyewe kwa wenyewe tangu kuzuka kwa vita hivyo mwezi Disemba mwaka 2013.

Akihojiwa na Idhaa hii kuhusu ujumbe wake kwa Baraza la Usalama, Bwana Ladsous amesema ni mambo kadhaa lakini Mosi..

(Sauti Ladsous)

"Dhahiri kabisa, hivi vita lazima vikome, kumekuwepo na machungu mengi nah ii haiwezi kuendelea! Pili suluhu la kisiasa sambamba na sitisho la mapigano linalotekelezeka lisongeshwe mbele kwa kasi.Tatu uwajibikaji ili wale ambao wanahusika na machungu haya lazima wawajibishwe na kile ambacho wamefanya.”

Tangu kuzuka kwa mapigano Disemba 2013, zaidi ya raia Milioni Mbili wa Sudan Kusini wamekimbia makwao ambapo 150,000 wamesaka hifadhi kwenye vituo vya hifadhi vya Umoja wa Mataifa.