Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani mashambulizi ya Boko Haram dhidi ya waislamu na wakristo

Ban alaani mashambulizi ya Boko Haram dhidi ya waislamu na wakristo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali mashambulio yaliyofanywa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram huko Cameroon, Niger, Nigeria na Chad ambapo ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na majeruhi wa tukio hilo.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Ban akitolea mfano wa mashambulizi yanayolenga waumini wa kikristo na wa kiislamu wakati wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kwenye majimbo la Borno na Yobe nchini Nigeria.

Amesema anatambua azma ya Rais Muhammadu Buhari ya kung’oa vitendo hivyo vya kidhalimu huku akipongeza nchi hizo ambazo zinaunda kamisheni ya bonde la Mto Chad na Benin kwa harakati zao za kukabiliana na Boko Haram.

Hata hivyo Ban amerejelea wito wake usaidizi rasilimali kama fedha na vifaa kwa kikosi cha pamoja cha kijeshi cha kudhibiti Boko Haram, MNJTF ili kiweze kuanza kazi zake kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu na ukimbizi.