Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upuuzaji wa haki, unyanyapaa vyashamirisha Ukimwi: Ban

Upuuzaji wa haki, unyanyapaa vyashamirisha Ukimwi: Ban

Ugonjwa wa Ukimwi unazidi kuwa janga na mateso kwa wengi duniani kutokana na sheria zilizopo pamoja na  unyanyapaa, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wakati akizindua ripoti ya Umoja huo kuhusu Ukimwi huko Bridgetown, Barbados.

Ripoti hiyo iitwayo kushinda ukimwi na kusongesha mbele afya duniani inatokana na mapendekezo kutoka kwa wataalamu wa afya, watu wanaoishi na Ukimwi, vijana,wanaharakati na wadau wa umoja wa Mataifa.

Ban amesema sheria duni na unyanyapaa vinasababisha watu wengi kutumbukia kwenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi na kukosa huduma za matibabu za kuokoa maisha yao akinukuu takwimu za Umoja wa Mataifa kuwa watu 250,000 huko Caribbean wanaishi na virusi vya Ukimwi.

Mathalani amesema chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja zinatishia haki zao za  binadamu na haki za afya akisema jamii ya kimataifa haiwezi kuvumilia ubaguzi huo kwa misingi ya jinsia ya mtu au utambulisho wake wa kijinsia.

Halikadhalika ametaka kuzingatiwa kwa haki za makahaba na wale wanaojidunga madawa ili kila mtu aweze kupata huduma dhidi ya Ukimwi wakati muafaka.

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa Ukimwi siyo tu suala la afya ya binadamu bali ni suala la msingi la haki za binadamu na hivyo utatokomezwa pale tu haki za msingi za kila mtu zitazingatiwa.