Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola: Tusibweteke la sivyo tutapoteza mafanikio yote: Ban

Ebola: Tusibweteke la sivyo tutapoteza mafanikio yote: Ban

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha wazi kisicho rasmi cha kupatiana taarifa kuhusu janga la kiafya lililotokana na mlipuko wa Ebola huko Afrika Magharibi.

Miongoni mwa taarifa zilizotolewa ni kuendelea kupungua kwa visa vipya vya Ebola huko Guinea na Sierra Leone wakati huu ambapo nchini Liberia ilitangazwa rasmi mwezi uliopita kuwa hakuna tena visa vipya.

Rais wa Baraza Kuu Sam Kutesa amesema mafanikio hayo yasisababishe jamii ya kimataifa ilegeze Kamba bali kuendeleza harakati na kuimarisha ufuatiliaji na mipango ya kujenga upya nchi hizo.

Ban Ki-moon ambaye alikuwa ni mmoja wa wazungumza alisema ujumbe wake ni tahadhari ya kwamba..

“Naleta ujumbe wetu wa hadhari. Ulimwengu umeungana kutokomeza mlipuko huu. Lakini uwekezaji wetu na kujitoa kwetu kutapotea iwapo hatutakamilisha kazi.:

Hivyo akatoa rai..

“Nalishi Baraza Kuu kuendelea kulipatia suala hili uzito wa kisiasa. Halikadhalika wahisani nawasihi waendelee na michango yao. Kupoteza usaidizi na msisitizo hivi sasa itakuwa ni janga.”

Hadi tarehe Mosi mwezi huu, Ebola ilikuwa imekumba wagonjwa 27,055 ambapo kati ya 11,142 wamefariki dunia wengi katika nchi za Liberia, Sierra Leone na Guinea tangu ugonjwa uibuke mwezi Machi mwaka jana.