Dhuluma kwa watoto Asia-Pasifiki inagharamu dola bilioni 209 kila mwaka- UNICEF
Dhuluma na ukatili dhidi ya watoto unazigharimu nchi za Asia Mashariki na Pasifiki takriban dola bilioni 209 kila mwaka, ikiwa ni sawa na asilimia 2 ya mapato ya jumla ya ukanda huo, imesema ripoti mpya ya Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF.
Kwa mujibu wa taarifa ya UNICEF, hii ndiyo mara ya kwanza tathmini ya gharama ya dhuluma dhidi ya watoto imefanywa katika ukanda huo, ikitokana na utafiti uliofanywa na timu ya wataalam wa kimataifa wakitumia mbinu zilizowahi kutumiwa katika nchi za Australia na Marekani.
Mkurugenzi wa UNICEF kwa ukanda huo, Daniel Toole, amesema kuwa inajulikana wazi kuwa ukatili dhidi ya watoto ni mbaya kimaadili, akiongeza kuwa utafiti huo unaonyesha kuwa kutochukua hatua dhidi ya ukatili huo kuna gharama kubwa kiuchumi kwa nchi na jamii za watu wake.
Amesema serikali zinapaswa kuchukua hatua ili kuwalinda watoto dhidi ya ukatili, siyo tu kwa ajili ya maslahi ya watoto, lakini pia kwa ajili ya vizazi vijavyo.