Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ahutubia bunge la EU azungumzia masuala ya wahamiaji kupitia Mediteranea na Andaman

Ban ahutubia bunge la EU azungumzia masuala ya wahamiaji kupitia Mediteranea na Andaman

Akiwa ziarani barani Ulaya, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amehutubia bunge la Muungano wa Ulaya, EU akigusia dhima muhimu ya chomboh icho katika kushamirisha ajenda ya umoja huo ikiwemo amani, maendeleo na  haki za binadamu.

Katika muktadha huo Ban akasisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto za wahamiaji wanaohatarisha maisha yao na kuvuka bahari za Mediteranea na Andamana ili kuokoa maisha yao.

Amesema maelfu ya wanawake, watoto na wanaume wanapoteza maisha yao akitolea mfano kupitia bahari ya mediteranea ambako mwaka huu pekee watu 1,800 wamefariki dunia baada ya kuzama ikiwa ni ongezeko mara 20 ikilinganishwa na mwaka jana.

Katibu Mkuu amesema nusu ya wanaovuka bahari hiyo wanakimbia mateso huko makwao na hivyo wanakidhi vigezo vya kupatiwa hifadhi na kwamba kuokoa maisha ni lazima kiwe kipaumbele cha juu.

Hivyo Ban akasema…

(Sauti ya Ban)

“Wakati tunahitaji kuona usimamizi zaidi wa sheria na hatua dhidi ya wasafirishaji haramu wa binadamu, tunahitaji pia mbinu mbadala na salama za safari hizi hatari sambamba na njia halali za uhamiaji, ikiwemo vibali vya kuishi ugenini kwa lengo la kukutanisha familia, ajira na masomo.”

Katibu Mkuu amesema chanzo cha uhamiaji kinapaswa kushughulikia, sambamba na unyanyapaa na ubaguzi wanaokumbana nao wahamiaji kwenye makazi mapya wanayohamia.