Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Brown apazia sauti mfuko wa kibinadamu kwa elimu ya watoto kwenye dharura

Brown apazia sauti mfuko wa kibinadamu kwa elimu ya watoto kwenye dharura

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Gordon Brown, ametoa wito kwa serikali ziafikie mara moja mfuko wa kimataifa wa kibinadamu kwa ajili ya elimu ya watoto katika hali za dharura, wakati mwaka huu ukionekana kuwa mbaya zaidi katika ukiukwaji wa haki za watoto.

Akiongea mbele ya waandishi wa habari mjini New York, Brown ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza ametoa wito kwa mashirika muhimu duniani na wadau wa maendeleo kuendeleza msukumo wa kongamano la dunia kuhusu elimu ambalo limehitimishwa nchini Korea Kusini, ili uafikiwe mfuko huo wa kibinadamu wa elimu wakati wa mkutano utakaofanyika mjini Oslo, Norway, kuanzia Julai 6 hadi 7 2015.

Amesema uwepo wa mfuko huo utaondoa kuchelewa kuchukua hatua za haraka iwapo majanga yanatokea na kuvuruga mwelekeo wa masomo wa watoto akitolea mfano Nepal ambako matetemeko ya ardhi yameharibu shule.

“Tungaliweza kukarabati shule hizi haraka, tungaliweza kushirikiana na mamlaka kwenye eneo hilo kufanya hilo iwapo tungalikuwa na mfuko wa kibinadamu wa elimu ambako tungepata pesa mara moja badala ya kusubiri na kuanza kupitisha bakuli kuomba omba tukisubiri fedha hizo. Ombi la dharura limetolewa la dola Milioni 21 na Umoja wa Mataifa lakini hadi wiki chache zilizopita imepatikana asilimia 1.5 tu.”

Iwapo makubaliano kuhusu mfuko huo yatafanywa, basi utazinduliwa baadaye mwaka huu kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.