Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la Elimu Duniani lapitisha azimio kuhusu mustakhbali wa elimu

Kongamano la Elimu Duniani lapitisha azimio kuhusu mustakhbali wa elimu

Azimio linalolenga kubadilisha mustakhbali wa elimu katika kipindi cha miaka 15 ijayo limepitishwa leo mwishoni mwa Kongamano la Elimu Duniani, mjini Incheon, Jamhuri ya Korea. Amina Hassan na maelezo kamili.

(TAARIFA YA AMINA)

Azimio hilo la Incheon limekaribishwa na jamii ya elimu duniani, wakiwemo mawaziri wa elimu kutoka zaidi ya nchi 100, mashirika yasiyo ya kiserikali na makundi ya vijana.

Azimio hilo linatoa msukumo kwa nchi zitoe fursa bora za elimu ambazo ni jumuishi, na zenye kuendeleza usawa kwa wote. Azimio hilo linatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya malengo ya elimu katika malengo ya maendeleo endelevu, ambayo yataridhiwa mnamo mwezi Septemba kwenye Umoja wa Mataifa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Irina Bokova, amesema azimio hilo ni hatua muhimu kwenda mbele, na kwamba inaashiria ari ya kutaka kuhakikisha kuwa watoto wote na vijana wanapokea mafunzo na stadi wanazohitaji ili kuishi kwa hadhi, kutimiza uwezo wao na kuchangia jamii zao kama raia wenye kuwajibika.