Baraza la Usalama lakaribisha tangazo la mazungumzo ya kisiasa Yemen

20 Mei 2015

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamekaribisha tangazo la Katibu Mkuu la kuandaa kongamano litakalowaleta wadau wote kuhusu Yemen mjini Geneva mnamo Mei 28, likilenga kuafikia suluhu la kisiasa kwa mzozo uliopo Yemen.

Wanachama hao wa Baraza la Usalama wamekariri kuwa mazungumzo jumuishi ya kisiasa yanayoandaliwa na Umoja wa Mataifa ni lazima uwe mchakato unaoongozwa na Wayemen wenyewe.

Akisoma ujumbe wa Baraza hilo mbele ya waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Balozi Raimonda Murmokaitë wa Lithuania ambaye ni rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Mei amesema:

“Wanachama wa Baraza la Usalama wamekariri wito wao kwa pande zote Yemen kuhudhuria mazungumzo haya na kushiriki bila masharti na kwa nia njema, kupinga vitendo vyote vya ghasia kwa minajili ya kufikia malengo ya kisiasa, na kujiepusha na uchochezi na vitendo vinavyoweza kuvuruga mpito wa kisiasa.”

Wajumbe wa Baraza la Usalama pia wamekaribisha habari kuwa watoaji misaada ya kibinadamu wa kimataifa waliweza kufikisha misaada muhimu kwa raia wanaoihitaji wakati wa sitisho la mapigano hivi karibuni, na kuunga mkono wito wa Katibu Mkuu wa kurejelea sitisho la mapigano kwa sababu za kibinadamu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud