Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo Burundi, Ban azungumza na Rais Kenyatta, kuzungumza pia na Rais Nkurunzinza

Mzozo Burundi, Ban azungumza na Rais Kenyatta, kuzungumza pia na Rais Nkurunzinza

Umoja wa Mataifa umeendelea na harakati za kusaka suluhu kwenye mzozo unaoendelea nchini Burundi ambapo hatua za hivi karibuni zaidi ni kutoka kwa Katibu Mkuu wa umoja huo Ban Ki-moon za kuzungumza kwa njia ya simu na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kuhusu kinachoendelea kwenye nchi hiyo ya Maziwa Makuu.

Ripoti hizo ni kwa mujibu wa Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq alizotoa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mjini New York, Marekani ambapo amesema katika mazungumzo na Rais Kenyatta…..

(Sauti ya Farhan)

“Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa viongozi kwenye ukanda huo kuunganisha jitihada zao kusaidia kusuluhisha mzozo wa Burundi. Wamekubaliana juu ya umuhimu wa mashauriano shirikishi. Katibu mkuu amepanga kuzunguzma na Rais Nkurunzinza na viongozi wengineo katika siku zijazo.”

Halikadhalika Farhan amesema mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa maziwa makuu, Said Djinnit leo yuko Bujumbura na taarifa zaidi kuhusu matokeo  ya ziara hiyo zitatolewa kadri zitakavyopatikana.