Viongozi Burundi jiepusheni na visasi: Ban
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito wa utulivu nchini Burundi huku akitaka viongozi wa kisiasa na usalama kukataa ghasia na vitendo vya kulipiza kisasi.
Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Ban akitoa kauli hiyo huku akielezea wasiwasi wake mkubwa juu ya kile kinachoendelea Burundi hivi sasa tangu kutangazwa kwa uteuzi wa Rais Pierre Nkurunzinza kuwania nafasi ya urais na tangazo la jaribio la mapinduzi tarehe 13 mwezi huu.
Katibu Mkuu ametaka kuheshimiwa kwa katiba ya Burundi sanjari na makubaliano ya Arusha yaliyorejesha amani nchini humo baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Amesisitiza kuwa yeyote ambaye anaagiza kufanyika kwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu atawajibika na hivyo amesema ana imani kubwa kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litazingatia njia mbali mali za kuchunguza kinachoendelea Burundi ikiwemo uwajibishaji.
Kwa mantiki hiyo amekumbusha mamlaka za Burundi umuhimu wa kulinda raia wote pamoja na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na ofisi zake.
Halikadhalika Ban ametumia fursa hiyo kupongeza Jumuiya yaAfrika Mashariki kwa uongozi wake kwenye suala la Burundi akisema anawasiliana kwa karibu na viongozi wa ukanda huo.
Amesema Umoja wa Mataifa kupitia mjumbe wake wa maziwa makuu Said Djinnit, utaendelea kushirikiana na EAC na Muungano wa AFrika kupatia suluhu mzozo wa Burundi huku akisihi raia wa nchi hiyo kuweka mazingira salama ya kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki haraka iwezekanavyo.