Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji: "Mapendekezo ya makazi mapya ni mwanzo mzuri lakini bado haitoshi" - UM

Wahamiaji: "Mapendekezo ya makazi mapya ni mwanzo mzuri lakini bado haitoshi" - UM

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wahamiaji François Crépeau, ameelezea matumaini na masikitiko yake kuhusu ajenda mpya ya Muungano wa Ulaya iliyozinduliwa na tume ya Ulaya ili kukabiliana na tatizo la wahamiaji barani humo.

Bwana Crépeau amesema mapendekezo ya makazi mapya ni mazuri kimsingi lakini haitoshi kulingana na ukubwa wa tatizo. Mipango inajumuisha makazi maalumu kwa ajili ya wakimbizi mradi ambao amekuwa akiupigia upatu tangu Septemba 2014.

Amesema idadi ya makazi haitoshi akisistiza kuwa majengo 20,000 kwenye Muungano wa Ulaya hayaendi sanjari na hali sasa ambayo mwaka 2014 imeshuhudia wahamiaji zaidi ya 200,000, ambapo wengi wao ni waoomba hifadhi wanaowasili Ulaya kwa boti.

Wahamiaji zaidi ya 60,000 wengi wao wakiwa waoomba hifadhi wameokolewa mwaka huu pekee amesema mwakilishi huyo.