Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lajadili hali ya Burundi

Baraza la usalama lajadili hali ya Burundi

Kufuatia sintofahamu iliyokumba Burundi, Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linakuwa na mashauriano ili kupata hali ilivyo hivi sasa kwenye nchi hiyo ya ukanda wa maziwa makuu barani Afrika. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Kikao hicho kinachofanyika kwa faragha kimeitishwa kwa ombi la Ufaransa wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa ulishasema unafuatilia kwa makini kinachoendelea nchini humo.

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa maziwa makuu, Said Djinit atahutubia kikao hicho kwa njia ya video kutoka Dar es salaam, Tanzania ambako alihudhuria kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki siku ya Jumatano kilichojadili hali ya Burundi.

Siku ya Jumatano baada ya ripoti za kuwepo kwa jaribio la mapinduzi nchini Burundi, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alinukuliwa akisema kuwa ..

(Sauti ya Dujarric)

“Unajua sidhani kama kuna mtu anafurahia au anatambua mapinduzi ya kijeshi ambayo ni uondoaji serikali madarakani kinyume cha katiba. Nadhani tuanchofahamu sasa hali inazidi kuwa ya mashaka, tunajaribu kupata taarifa ili tufahamu kinachoendelea Bujumbura. Nadhani inazidi kubainika kuwa mara kwa mara katibu mkuu amesisitiza siyo tu kwa nchi za Afrika bali pia kwingineko duniani juu ya umuhimu wa viongozi kusikiliza matakwa ya wananchi wao na kuheshimu taasisi za kidemokrasia. Bila shaka hali Burundi inabadilika hivyo tuendelea kufuatilia kwa karibu sana.”