Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaohitaji misaada ya kibinadamu Iraq wazidi milioni 8- OCHA

Wanaohitaji misaada ya kibinadamu Iraq wazidi milioni 8- OCHA

Mratibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura, Valerie Amos, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, idadi ya raia wa Iraq wanaohitaji misaada ya kibinadamu imeongezeka hadi milioni 8.2, likiwa ni ongezeko la watu milioni 3 katika kipindi cha miezi mitano.

Akizungumza wakati Baraza hilo likikutana kujadili kuhusu ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, UNAMI, Bi Amos amesema kwamba nusu ya watu waliolazimika kuhama makwao ni watoto, na kwamba mikoa yote 18 nchini Iraq imeathiriwa. Iraq pia bado inawapa hifadhi wakimbizi 250,000 wa Syria.

“Migogoro, mashambulizi yanayolenga raia na vitisho kwa misingi ya kikabila na kidini, vinaendelea kuiathiri nchi hiyo. Kuwalazimu watu kuhama kunaendelea kila uchao, watu 120,000 wakiwa wamelazimika kuhama kutoka Ramadi kwenye mkoa wa Anbar mwezi uliopita- kiashiria cha hali ilivyo tete nchini Iraq.”

Bi Amos amesema, kadri kipindi cha mgogoro nchini Iraq kinavyoongezeka, ndivyo hali ya dharura inavyozidi kuongezeka pia.

“Familia haziwezi tena kujikimu. Rasilmali za jamii zinazowapa hifadhi zimekwisha. Utoaji huduma za kijamii na miundo mbinu imezidiwa. Umaskini na ukosefu wa ajira vimeongezeka, huku gharama ya maisha ikipanda. Familia zilizolazimika kuhama hivi karibuni zinapata ugumu kupata maeneo salama nchini ambako zinaweza kupata hifadhi wanayohitaji.”

Mkuu huyo wa OCHA amesema pia kuwa, anahofia hatma ya mamilioni ya raia wa Iraq wanaoishi katika maeneo yaliyo nje ya udhibiti wa serikali, yakiwemo yaliyo chini ya ISIL, takriban mwaka mmoja tangu ISIL ilipoushambulia mji wa Mosul.