Skip to main content

Mwakilishi wa UM akutana na wadau katika harakati za kusaka amani Syria

Mwakilishi wa UM akutana na wadau katika harakati za kusaka amani Syria

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini Syria, Staffan de Mistura, amekutana na kufanya mashauriano wadau katika harakati za kutafutia suluhu mzozo wa Syria mjini Geneva, Uswisi.

Miongoni mwa alioukutana nao ni Mwakilishi wa Kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Alexey Borodavkin, ambaye alijadili naye njia za kuunga mkono pande husika katika mzozo wa Syria kuelekea kuanzisha mazungumzo ya amani, pamoja na mchango wa Umoja wa Mataifa, jamii ya kimataifa na mataifa ya kikanda katika juhudi hizo.

Bwana de Mistura pia amekutana na Mwakilishi wa Uingereza, Simon Gass, ambaye ameelezea tathmini ya serikali yake kuhusu hali nchini Syria na katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Pia amekutana na mjumbe wa muungano wa upinzani na vikosi vya mapinduzi nchini Syria,Haitham al-Maleh, ambaye aliwasilisha barua ya muungano huo, ikielezea msimamo wake kuhusu jinsi ya kuutatua mzozo wa Syria. Bwana de Mistura ameunga mkono mchango wa muungano huo wa upinzani katika mashauriano hayo ya Geneva.

Mwishoni mwa mikutano hiyo, de Mistura amesema mazungumzo ya leo na wawakilishi wa Syria na jamii ya kimataifa ni ukumbusho wa haja ya dharura ya pamoja ya kuwasaidia watu wa Syria kufikia suluhu la kisiasa na kuumaliza mzozo nchini humo.