Skip to main content

Ukosefu wa makubaliano ya amani Sudan Kusini ni kikwazo: Mkuu UNMISS

Ukosefu wa makubaliano ya amani Sudan Kusini ni kikwazo: Mkuu UNMISS

Licha ya kwamba hatuna mamlaka ya kuchagiza mchakato wa kisiasa nchini Sudan Kusini, ukosefu wa mwelekeo wa kufikia makubaliano hayo unatukwamisha harakati zetu.

Ni ujumbe wa Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, Ellen Margrethe Løj alipohutubia Baraza la Usalama wakati wa kikao kuhusu shughuli za ujumbe wa umoja wa mataifa Sudan Kusini,  UNMISS na kamati ya vikwazo dhidi ya nchi hiyo.

(Sauti ya Løj-1)

“Tulikuwa na matumaini makubwa ya kumaliza mkwamo mapema mwaka huu. Lakini nimesikitishwa sana na kitendo cha pande husika kushindwa kuafikiana. Hakuna mbadala wa kusitisha mapigano na kukamilisha mkataba wa amani ili Sudan Kusini iende kwenye mwelekeo wa amani na utulivu.”

Kuhusu usambazaji wa huduma zake, Bi. Løj  ambaye pia ni mkuu UNMISS amesema bado wanaendelea kukumbwa na vizuizi huku usalama wa watoa huduma za misaada ukiwa mashakani kwa kuwa..

(Sauti ya Bi. Løj)

“Kama ilivyoelezwa kweney ripoti ya katibu mkuu, wafanyakazi watatu wa WFP ambao ni raia wa Sudan Kusini ambao walipotea tarehe Mosi Aprili mwaka huu huko jimbo la Upper Nile hadi sasa hawajapatikana. Hali ya wafanyakazi watano wa Umoja wa Mataifa niliowarejelea kwenye hotuba yangu mwezi Oktoba wakiwemo wawili wasiojulikana waliko na watatu wanaoshikiliwa,  bado haijbadilika.”

Ametoa wito kwa Baraza la Usalama kuchukua hatua ili misimamo ya pande kinzani nchini Sudan Kusini iweze kulegezwa na amani na utulivu viweze kurejea.