Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wakimbizi wa Burundi yafikia 50,000:UNHCR

Idadi ya wakimbizi wa Burundi yafikia 50,000:UNHCR

Idadi ya wakimbizi wa Burundi waliokimbilia nchi jirani kufuatia ghasia zinazoendelea nchini mwao imeongezeka na kufikia Elfu Hamsini katika wiki moja iliyopita pekee.

Hiyo ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR ikisema raia hao wamekimbilia Rwanda, Tanzania na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo licha ya amani kutawala nchini humo tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2005.

Idadi kubwa ya wakimbizi wamekimbilia Rwanda na sasa Tanzania baada ya vizuizi vya kuingia kuondolewa na wengi wao ni wanawake na watoto wakikumbwa na madhila.

Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR, Geneva.

(Sauti ya Adrian)

“Wanawake wengi wameripoti kubakwa na watu wenye silaha na madhila mengine, wakihonga ili waweze kupita kwenye vizuizi barabarani. Wengine wametembea saa nyingi porini wakiwa na watoto wao. UNHCR inasihi mamlaka za Burundi kuruhusu watu watembee huru, ni muhimu mipaka ikabakia wazi.”

Wakati huo huo, shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema litahitaji dola Milioni Tano ili kukidhi mahitaji ya wakimbizi kati ya Elfu Hamsini na Laki Moja wa Burundi wanaokadiriwa kuwa wataingia nchini Rwanda kwa kipindi cha miezi Sita ijayo.