Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola Milioni Tano zahitajika kukidhi wakimbizi watarajiwa wa Burundi:WFP

Dola Milioni Tano zahitajika kukidhi wakimbizi watarajiwa wa Burundi:WFP

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limeelezea wasiwasi wake kuwa mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini Burundi unaweza kugeuka na kuwa wa kibinadamu kutokana na kasi ya makumi ya maelfu ya raia wanaozidi kukimbilia nchi jirani ikiwemo Rwanda.

Mathalani inasema nchini Rwanda tayari wanapatia msaada wa lishe zaidi ya wakimbizi 25,000 wa Burundi na idadi inaongezeka wakati huu ambapo shirika hilo na wadau wake wamejipanga kusaidia hadi wakimbizi Laki Moja nchini humo iwapo italazimika, lakini fedha hazitoshi.

Msemaji wa WFP huko Geneva, Elizabeth Byrs amesema wanahitaji dola Milioni Tano kukidhi mahitaji kwa wakimbizi ndani ya miezi sita ijayo..

(Sauti ya Elizabeth)

“WFP na wadau wake wanajianda kusaidia wakimbizi kati ya Elfu Hamsini hadi Laki moja nchini Rwanda iwapo itaonekana muhimu kufanya hivyo, lakini rasilimali zetu tayari zimezidiwa uwezo kutokana na wimbi la wakimbizi.”

Pamoja na wakimbizi wapya wa Burundi, Rwanda tayari inahifadhi wakimbizi zaidi ya Elfu Sabini na Tatu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.