Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Polisi na mahakama kandamizi ni kikwazo kwa jamii kuendelea:Ban

Polisi na mahakama kandamizi ni kikwazo kwa jamii kuendelea:Ban

Maelfu ya watu wanauawa kutokana na ghasia zihusianazo na madawa ya kulevya na ugaidi, zaidi ya wanawake 40,000 huuawa na wapenzi wao na vijana wanashindwa kujiendeleza kutokana na magenge ya uhalifu kwenye maeneo yao.

Hiyo ni sehemu ya hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyotoa wakati akifungua mkutano wa 13 kuhusu uzuiaji uhalifu na mfumo wa haki kudhibiti uhalifu huko Doha, Qatar leo akitanabaisha kiwango cha uhalifu duniani.

« Yawezekana vipi watu kushamiri kimaendeleo iwapo polisi na mahakama vinatumika kama vyombo vya kuwakandamiza ? maendeleo na haki za binadamu hutegemea mifumo ya kisheria inayoendeleza usawa na utawala bora unaoheshimu sheria hizo. Jamii zote zinahitaji mifumo ya mahakama inayozingatia haki, thabiti, inayowajibika na inayotoa haki kwa wote. »

Katibu Mkuu amesema uhalifu unatishia amani na usalama, unakwamisha maendeleo na kukiuka haki za binadamu hivyo akasisitiza umuhimu wa ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015 pamoja na nchi hizo kuridhia na kutekeleza mikataba dhidi ya madawa ya kulevya, uhalifu, rushwa na ugaidi akitaka nchi ziunge mkono juhudi zinazofanywa na ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu madawa ya kulevya na uhalifu, UNODC.

Kuhusu uhalifu mtandao Katibu Mkuu amesema..

“Uhalifu mtandao sasa umekuwa biashara ambayo inazidi mabiliono ya dola kila mwaka kupitia udanganyifu kwenye mitandao, wizi wa utambulisho wa mtu na kupotea kwa hakimiliki. Inaathiri mamilioni ya watu duniani kote, serikali na biashara.”

 Zaidi ya washirki 4,000 kutoka mataifa 142 wanashiriki mkutano huo ambao umekuwa wa aina yake kwa kuwa katika siku ya kwanza washiriki wameridhia azimio lake.

Azimio hilo pamoja na mambo mengine  linasisitiza mambo muhimu kuhusu udhibiti wa uhalifu unaovuka mipaka na na kuimarisha mifumo ya haki na uzuiaji wa uhalifu.