Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya mpito kuhusu Eritrea yabaini wazi mwelekeo wa ukiukaji wa haki:

Ripoti ya mpito kuhusu Eritrea yabaini wazi mwelekeo wa ukiukaji wa haki:

Ripoti ya mpito ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Eritrea imebaini bayana mwelekeo wa ukiukaji wa haki za binadamu.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa kwenye baraza la haki za binadamu inafuatia uchunguzi wa miezi minne uliofanywa na tume ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi wa haki za binadamu nchini Eritrea.

Wakati tume hiyo ilikataliwa fursa ya kuingia Eritrea mwenyekiti wake Mike Smith amesema imekusanya ushahidi kutoka kwa watu zaidi ya 500 raia wa Eritrea wanaoshi ughaibuni , maoni yanayoashiria ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Bwana Smith amesema vitu kama huduma ya jeshi ya kitaifa ni kwa watu wote na ni kwa muda usiojulikana. Kuanzia umri wa miaka 17 raia wa Eritrea wanaweza kujikuta maisha yao yote ni kutoa huduma katika jeshi la kitaifa , wakihangaika kuishi kwa chini ya dola mbili kwa siku.

Na hii kama haitoshi wanalazimika kutimiza mahitaji yao ya muhimu, na huku wakifikiria jinsi ya kuendesha familia zao. Ameongeza kuwa hali hiyo imewafanya raia wengi wa Eritrea kupoteza matumaini yoyote ya maisha ya baadaye.