Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Syria wamulikwa katika Baraza la Usalama

Mzozo wa Syria wamulikwa katika Baraza la Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo mchana limekutana kujadili hali Mashariki ya Kati, likimulika hasa hali nchini Syria, ambako mapigano yanaingia mwaka wa tano. Baraza hilo limesikia pia ripoti za wakuu wa mashirika mawili ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.

Msaidizi wa Katibu Mkuu na Naibu Mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu Kyung-wha Kang, amesema kuwa pande zinazozozana katika mzozo wa Syria zinaendelea kuwaua na kuwalenga raia na miundo mbinu ya raia, zikiwemo huduma muhimu kama vile maji na umeme, zikikiuka maagizo ya azimio 2139 na sheria ya kimataifa ya kibinadamu bila kujali. Amesema hali hii imewafanya raia kuendelea kuteseka

“Kati ya watu 212,000 walionaswa katika mzozo, katika hali ambayo inaendelea kuzorota kila siku, ni watu 304 ndio walioweza kufikiwa na msaada wa chakula mwezi Januari. Watu hao 304 walikuwa Yarmouk, ambako watu 18,000 hawana chochote. Katika maeneo mengine yaliyozingirwa, pande zinazozozana zimeendelea kuzuia ufikiaji wa raia. Wagonjwa au majeruhi kwa kawaida hawana mahali salama pa kupata matibabu.”

Naye Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Antonio Guterres, amekariri ujumbe alioutoa kwa Baraza la Usalama mnamo mwaka 2013 kuwa mzozo wa Syria ulikuwa umeibua tatizo baya zaidi la kibinadamu katika kizazi cha sasa, na kwamba unatishia amani na usalama wa kikanda na kimataifa.

“Iraq ilishuhudia kuvuka na kughubikwa kabisa na mzozo wa ndani ya nchi nyingine katika historia hivi karibuni. Lebanon imekuwa daima kwenye tahadhari kiusalama, na kumekuwa na vitisho vinavyoongezeka kwa Jordan miezi michache iliyopita. Halikadhalika, tatizo la wakimbizi wa Syria limezidi uwezo uliopo wa kukabiliana nalo, wakimbizi milioni 3.8 wakiwa wamesajiliwa katika nchi jirani.”

Amesema nchi za Lebanon na Jordan zimeshuhudia ongezeko la idadi ya watu katika miaka michache na kufikia kiwango ambacho zingeweza tu kufikia katika miongo kadhaa, akiongeza kuwa Uturuki sasa imekuwa ndiyo nchi yenye wakimbizi wengi zaidi duniani.

“Wingi wa wakimbizi umeathiri pakubwa uchumi na jamii za nchi za Lebanon, Jordan na Kaskazini mwa Iraq, na hivyo kuzidi uwezo wa huduma za kijamii, miundo mbinu na rasilmali za serikali. Usaidizi wa kimataifa haujaweza kulingana na ukubwa wa mahitaji.”

Guterres amesema anavunjwa moyo kama Kamishna Mkuu kuona familia za watu wa Syria zinazokimbia mzozo huo zikihatarisha maisha yao kwa boti zisizo salama ili kusaka hifadhi Ulaya, akitaka ziwekwe njia halali za wakimbizi hao kuomba hifadhi katika nchi za ng’ambo ili kupunguza hatari hiyo.