Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi sikilizeni wananchi la sivyo mwajiporomosha:Ban

Viongozi sikilizeni wananchi la sivyo mwajiporomosha:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema viongozi wanapaswa kusikiliza wananchi wao ili kuepusha hisia za ubaguzi zinazoibua misimamo mikali ndani ya jamii. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa viongozi wakuu wa serikali mjini Dubai, Falme za kiarabu.

Ban amesema duniani kote hivi sasa wananchi wanataka uwazi wa serikali zao na iwapo viongozi watajiona wao ni bora kuliko sheria basi wanatumbukiza serikali zao katika hatari ya kuporomoka.

Amesema ufisadi, matumizi mabaya ya taasisi za umma huchochea vurugu na ukosefu wa utulivu akisema utulivu wa dhati unataka taasisi zinazoaminika na zinazohudumia watu wote kwa usawa akigusia pia wanawake ambao kwa kipindi kirefu sauti zao zimekuwa zikipuuzwa licha ya kuwa ni nusu ya idadi ya watu wote duniani.

Kwa mantiki hiyo amesifu serikali ya Saudia kwa kutangaza mwaka wa 2015 kuwa wa ubunifu akisema kwa Umoja wa Mataifa ni mwaka wa kuchukua hatua za mabadiliko ili kuwa na dunia endelevu, amani na usawa kwa wote.

 

Amezitaka serikali kushirikisha zaidi wananchi katika kusaka suluhu za changamoto za maendeleo na akidokeza kuwa serikali zinapokuwa za uwazi kwa umma, zinaaminika na hiyo ni muhimu kwa kujenga jamii na nchi thabiti.