Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nigeria hakikisha kila mwenye haki anapiga kura:Ban

Nigeria hakikisha kila mwenye haki anapiga kura:Ban

Kufuatia uamuzi wa Tume ya uchaguzi nchini Nigeria kuahirisha uchaguzi mkuu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amekisihi chombo hicho kuchukua hatua zote za lazima kuhakikisha watu wote wenye haki ya kupiga kura wanafanya hivyo.

Ban amesema hayo katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake ikieleza kutambua kwake kuahirishwa kwa uchaguzi huo uliokuwa ufanyike tarehe 14 mwezi huu ambapo sasa uchaguzi umepangwa kufanyika tarehe 28 mwezi Machi 2015.

Ametaja hatua hizo muhimu za kuchukuliwa kuwa ni pamoja na kusambaza haraka kadi za kudumu za wapiga kura kwa wale ambao wana haki na walikuwa hawajapatiwa hata waliokimbia makazi yao ili waweze kutekeleza haki yao ya msingi.

Katibu Mkuu pia amekuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na wagombea urais Rais Goodluck Jonathan na Muhammad Buhari kutoka upinzani ambapo amewasihi wote kuzingatia makubaliano ya Abuja ambayo waliridhia kwa lengo la kuepusha ghasia wakati wa uchaguzi.

Amesema ni matarajio yake kuwa mamlaka za Nigeria zitahakikisha uchaguzi unafanyika bila vurugu na kuweka hatua za kutosha za usalama ili wapiga kura nchini kote Nigeria waweze kufanya hivyo kwa usalama na bila hofu.

Ban amesema mafanikio ya uchaguzi huo yataimarisha demokrasia na kuwezesha Nigeria kuwa na dhima ongozi ya kuendelea amani na usalama kwenye kanda yake.