Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya mkwamo dhidi ya Ebola, WHO yataka hatua:

Licha ya mkwamo dhidi ya Ebola, WHO yataka hatua:

Shirika la afya duniani, WHO limetoa ripoti yake kuhusu hali ya mlipuko wa Ebola huko Afrika Magharibi inayoonyesha kuongezeka kwa mara ya kwanza kwa visa vipya vya Ebola mwaka huu wa 2015.

Ripoti hiyo inasema kwa ujumla visa vipya vimeongezeka na kufikia 124 huko Guinea, Liberia na Sierra Leone kwenye wiki inayoishia tarehe Mosi Februari ikilinganishwa na visa chini ya 100 wiki iliyotangulia.

Mwitikio hasi wa jamii dhidi ya Ebola, kuenea kwa mlipuko kwenye eneo kubwa huko Guinea na kusambaa kwa kirusi huko Sierra Leone ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha mafanikio ya kudumu dhidi ya kirusi hicho hatari.

WHO inasema kadri msimu wa mvua unavyokaribia, ni vyema kuchukua hatua za dharura kumaliza mlipuko hususan kwenye maeneo yaliyo vigumu kufikika.