Mapigano yaliyochacha Ukraine yamesababisha vifo vingi: UM

23 Januari 2015

Kwa mujibu wa Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, kuongezeka kwa mapigano ya hivi karibuni nchini Ukraine kumesababisha vifo zaidi vya raia kuliko wakati mwingine tangu kusainiwa kwa mkataba wa kusitisha mapigano mwaka jana.

Mapigano nchini Ukraine tangu Januari 13 yamesababisha jumla ya vifo vya raia wapatao 5,086 na kuna huenda idadi halisi ikawa ni ya juu zaidi, kwa mujibu wa msemaji wa ofisi ya haki za binadamu, Rupert Colville,

“Katika siku tisa tu, kati ya tarehe 13 na 21 Januari, watu wapatao 262 waliuawa kutokana na vita. Hii ikiwa ni kwa wastani watu angalau 29 kila siku na hivyo hiki kimekuwa kipindi ambapo kumekuwa na vifo vingi zaidi tangu kutangazwa kusitishwa kwa mapigano tarehe 5 Septemba”

Aidha, Bw. Colville amewaambia waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi kuwa watu wengine 10, 948 wamejeruhiwa katika kipindi hicho tangu makubaliano ya Minsk yaliposainiwa Septemba mwaka jana.

Hali hiyo inakuja huku kukiwa na mapigano makali katika eneo la Donetsk mashariki mwa Ukraine, hasa karibu na uwanja wa ndege.

Wapiganaji wa serikali na wapiganaji wanaoungwa mkono na Urusi wameripotiwa kutumia mizinga mizito wakati wa mapigano hayo katika miji kadhaa ya ukanda wa Luhansk.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter