Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto walemavu wametumiwa katika mashambulizi ya kigaidi Iraq- ripoti

Watoto walemavu wametumiwa katika mashambulizi ya kigaidi Iraq- ripoti

Ukiukaji wa haki za watoto unaendelea nchini Iraq, ambako watoto walemavu wanaendelea kutumiwa kufanya mashambulizi ya kigaidi, kwa imani kuwa wataweza kupona.

Katika ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Iraq, wataalam wa haki za binadamu wameelezea pia kwa kina kuhusu kutumia watoto katika biashara ya ngono na kutengeneza picha na filamu za ngono, pamoja na vitendo vingine katili vinavyowalenga watoto wa kike, kama vile ukeketaji, ndoa za utotoni na za lazima, na uhalifu mwingine.

Ripoti hiyo imechapishwa kama sehemu ya tathmini ya kila mwaka ya Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za mtoto, ambayo inakutana mjini Geneva, Uswisi, ikimulika sera za nchi 12 kuhusu haki za mtoto.

Wataalam walioichangia ripoti hiyo wamesema matatizo mengi ya Iraq yalikuwepo hata kabla ya uvamizi wa kundi la kigaidi linalotaka kuweka dola la Uislamu wenye msimamo mkali, ISIL, mnamo mwaka 2014.