Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huko CAR hali ya watoto taabani:UNICEF

Mtoto katika kambi ya wakimbizi ya M'Poko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. (Picha:UN/Catianne Tijerina)

Huko CAR hali ya watoto taabani:UNICEF

Mwaka mmoja baada ya mapigano makali huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, hali ya watoto inazidi kuwa taabani ambapo watoto wawili kati ya watano wanakabiliwa na mahitaji ya dharura.

Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kanda ya Afrika Magharibi na Kati, Manuel Fontaine amesema hali hiyo inatokana na ukosefu wa fedha na usalama wa watoa huduma za misaada.

Mathalani amesema mashambulizi dhidi ya wafanyakazi hao sambamba na uporaji wa vifaa tiba umesababisha watoto wakose huduma muhimu za afya, maji, elimu na ulinzi.

Fontaine amesema kuibuka kwa mizozo kwingineko duniani kumesahaulisha jamii ya kimataifa suala la watoto wa CAR licha ya kwamba watoto zaidi ya Milioni 2.5 nchini humo wanaishi maisha ya woga kila uchao.

Ameomba jamii ya kimataifa wakati inajiandaa kusherehekea mwaka mpya itumie fursa hiyo kutoa usaidizi kwa ajili ya mustakhbali bora wa watoto wa CAR.